Jumanne, 11 Juni 2013

KIEMBA ASAINI MKATABA MIAKA 2 SIMBA SC

BREAKING NEWS; AMRI KIEMBA ASAINI MKATABA MIAKA 2 SIMBA SC LEO HII

Hadi 2015 Msimbazi; Amri Kiemba amesaini miaka miwili leo Simba SC
Na salum amry
HATIMAYE kiungo Amri Ramadhani Kiemba amesaini Mkataba mpya na Simba SC mchana wa leo kuendelea kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili, hivyo kuzima tetesi kwamba alikuwa mbioni kurejea klabu yake ya zamani Yanga SC.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY mchana huu, Kiemba amesema amesaini mbele ya Kaimu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ mchana huu.
“Unajua mimi si muongeaji, wakati magazeti yanaandika mimi nimesaini Yanga nilikuwa nashangaa sana. Ila sikutaka kujibu, sasa ukweli ni huu nakupa Bin Zubeiry, nimesaini Simba kwa miaka miwili zaidi,”alisema.
Amesema kwa sasa anaelekeza nguvu zake katika kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars na anaamini mjadala wa Kiemba umekwisha salama, sasa ni zamu ya wengine.
Kiemba amesaini SImba SC leo ikiwa ni siku moja tu tangu arejee nchini kutoka Morocco alipokuwa na timu ya taifa, Taifa Stars.
Kiemba yuko juu kwa sasa kisoka na alikuwa lulu Morocco kutokana na kuifungia Tanzania, Taifa Stars bao la kufutia machozi ikilala 2-1 mbele ya wenyeji, Simba wa Atlasi Jumamosi Uwanja wa Marakech, Morocco.
Baada ya mchezo huo, mashabiki wa soka Morocco walianza kumfuatafuata Kiemba wakiomba kupiga naye picha na walimtambua rahisi kwa sababu ya rasta zake.
Kiemba aliendelea kusumbuliwa na Wamorocco hadi hotelini Pullman Stars ilipifikia na hadi wakati Stars inaondoka Marakech, madereva teksi wa hotelini hapo, walimuomba kupiga naye picha.
Hali hiyo iliendelea hadi Stars ilipotua Casablanca kwa ajili ya kupanda ndege kurejea Dar es Salaam na Kiemba hakuwafanyia hiana aliwapa ushirikiano na kwa ujumla Waarabu walimfuruhia mno kiungo huyo.
Kabla ya mchezo, mchezaji ambaye Waarabu walikuwa wanamtaja na kumuulizia sana alikuwa Mbwana Ally Samatta aliyewafunga mabao mawili katika ushindi wa Stars wa 3-1 Dar es Salaam.
Pamoja na Kiemba na Samatta, Waarabu wa Morocco wameiheshimu timu nzima ya Tanzania kwa mchezo uwezo wake kisoka na kusema ina vipaji vingi, Thomas Ulimwengu, Frank Domayo, Salum Abubakar na Shomary Kapombe wakiwa wachezaji wengine waliowachengua zaidi.
Stars ilifungwa 2-1 na wenyeji Jumamosi katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani.
Hadi mapumziko, Morocco walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Abderazak Hemed Allah dakika ya 37, baada ya yeye mwenyewe kujiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kugongana na Aggrey Morris.
Morris alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya hapo na Stars wakabaki pungufu.
Dakika ya 25 Thomas Ulimwengu alifanya kazi nzuri ya kumtoka beki, lakini shuti lake likadakwa na kipa.
Kocha Kim Poulsen aliwapumzisha kwa mpigo washambuliaji Mrisho Ngassa na Ulimwengu dakika ya 44 na kuwaingiza beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’.
Kipindi cha pili Morocco walirejea na moto tena, wakiishambulia zaidi Stars iliyoonekana kudhoofika na katika dakika ya 50 Youssef El Arabi akafunga bao la pili kiulaini baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania na kubaki na kipa Juma Kaseja.
Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza liliipatia Stars bao la kwanza dakika ya 61 lililofungwa na Amri Kiemba kwa shuti la mbali kutoka wingi ya kushoto.
Dakika ya 82 Kim alimpumzisha Vialli na kumuingiza John Bocco ‘Adebayor’ ambaye aliongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Kwa matokeo hayo, Stars inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili nyumbani na kufungwa mbili zote ugenini, nyingine ikiwa dhidi ya Ivory Coast.
Lakini Stars inabaki nafasi ya pili mbele ya Morocco yene pointi tano sasa, wakati Ivory Coast wanaongoza kwa pointi zao 10.

Jumamosi, 8 Juni 2013

NI MDOGOLAKINI NI MACHACHARI


Beki huyo ameonyesha kuwa ni hodari wa kucheza mipira ya kichwa kwa kuzuia na kushambulia kutafuta mabao kama kona na krosi ingawa wasiwasi uliopo kwa mashabiki wa klabu hiyo ni udogo wa umbile lake.
 
UKIMUONA umbo lake unaweza kumuona wa kawaida sana, ni umbo ambalo halitishi. Si mrefu sana, si mpana sana ni mchezaji wa wastani tu, lakini shughuli yake isubiri uwanjani.
Mmoja wa wachambuzi mahiri na Mhariri wa Michezo wa Gazeti Kuu nchini Uganda la New Vision Fred Kaweesi alipoisoma Mwanaspoti na kusikia beki Samweli Ssenkoomi amesaini Simba alitamka maneno machache; “Simba wamepata mtu, huyo jamaa mzuri sana ila wasimpe presha bado mdogo sana. Wampe nafasi atumie akili yake.”
Simba imemsajili beki huyo wa Uganda kutoka URA kwa mkataba wa miaka miwili kwa lengo la kuimarisha safu ya beki ya kati ambayo iliyumba msimu uliopita na hata kwenye ripoti yake kocha aliyeachana na Simba, Mfaransa Patrick Liewig alishauri asajiliwe beki wa kati mzoefu. Alitua nchini usiku wa Jumatatu akitokea kwao Uganda na kuanza mazoezi ya pamoja na Simba Jumanne jioni wiki hii.
Akiwa katika mazoezi hayo, Ssenkoomi ameonyesha kuwa ni mjanja uwanjani na ana uamuzi wa haraka na uwezo mkubwa wa kupanda kushambulia mbele, pia ni mwepesi wa kushuka kuzuia.
Beki huyo ameonyesha kuwa ni hodari wa kucheza mipira ya kichwa kwa kuzuia na kushambulia kutafuta mabao kama kona na krosi ingawa wasiwasi uliopo kwa mashabiki wa klabu hiyo ni udogo wa umbile lake kwa sababu hamtishi straika ila ana akili na anajua anachokifanya.
Mwanaspoti ilizungumza naye akasema; “Nimeamua kuja Simba kwa lengo moja la kutimiza kile wanachokikusudia kwa kuhakikisha nacheza kwa ubora na kuifanya timu ing’are,”anasema Ssenkoomi ambaye anaishabikia klabu ya Real Madrid ya Hispania inayofikiria kumpa ukocha Zinedine Zidane.
“Lakini pia kwangu ni hatua moja, nina malengo ya kucheza Ulaya, kuja kwangu Simba nafungua njia kwa ajili ya kukamilisha ndoto zangu hizo. Naamini nitafanya kile ninachokikusuadia tena kizuri zaidi kubwa nahitaji ushirikiano kutoka kwa wachezaji wanzangu, benchi la ufundi na mashabiki kwa ujumla,”anafafanua Ssenkoomi aliyeweka wazi tayari amesaini mkataba wa miaka miwili na hakuja Tanzania kukaa benchi kwavile anataka kung’ara zaidi ya Joseph Owino beki wa Uganda aliyeondoka Simba.
Hata hivyo Ssenkoomi ametoa angalizo kwa kuwaomba mashabiki wampe muda kwani anatoka kwenye mapumziko na hajafanya mazoezi kwa kipindi kirefu.
“Ninatoka kwenye mapumziko, sijacheza kwa kipindi kirefu, ni ugumu ambao unanitatiza hata hivyo nitafanya kitu kitakachowafurahisha benchi la ufundi na mashabiki kwa ujumla,”anasema mchezaji huyo ambaye baada ya mazoezi ya kwanza na Simba alilalamikia uchakavu wa Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
“Kitu kingine ni ubovu wa sehemu ya kuchezea ndani, hali ya uwanja si nzuri imekuwa ikinipa wakati mgumu kucheza. Ushindani upo kila mahali, nimefurahi kukutana na wachezaji mbalimbali na kwa kipindi kifupi nimependa ushirikiano wao,”anasema na kuongeza kuwa amezoea mazingira ya Afrika Mashariki hivyo hadhani kama Tanzania itampa shida kwavile haitofautiani na Uganda.
“Wachezaji wazuri ambao kwangu ni changamoto na mambo mengine ni mimi mwenyewe katika kujituma, kufahamu majukumu yangu ninayopewa na mwalimu,” anaongeza mchezaji huyo ambaye Mwanaspoti linajua amependekezwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Simba, Mosses Basena ambaye ni raia wa Uganda.
Basena amewaambia viongozi kwamba mchezaji huyo ni mzuri na anaweza kufanya kazi kubwa kwenye ufundi ingawa habari za ndani zinadai kiungo wa TP Mazembe, Patrick Ochang anaomba kila kukicha arudi Msimbazi baada ya kupoteza namba katika kikosi cha wachezaji 18 wa kwanza Mazembe hivyo kumfanya kupoteza posho na masilahi manono.

TUIOMBEE TAIFA STARS




TAIFA STARS inacheza mechi ya pili ya mchujo ya Kombe la Dunia ugenini leo Jumamosi dhidi ya wenyeji Morocco ‘Lions of the Atlas’ huku ikipania kupata matokeo mazuri.
Mechi hiyo ya nne kwa Taifa Stars katika michuano hiyo hatua ya makundi inachezwa saa 3:00 usiku kwa saa za hapa, ambapo kwa Tanzania itakuwa saa 5:00 usiku kwenye Uwanja wa Grand Stade, mjini Marrakech.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema timu yake inatarajia kucheza vizuri lengo likiwa ni kuhakikisha inapata matokeo baada ya dakika 90 za mechi hiyo itakayochezeshwa na Daniel Frazier Bennett kutoka Afrika Kusini.
“Unapocheza ugenini ni lazima uwe makini na mwangalifu. Usiruhusu mpinzani wako akakuvuruga hasa dakika 20 za mwanzo. Lengo letu kuja hapa ni kufanya vizuri, na tumejiandaa kimwili na kiakili,” alisema Kim ambaye ameiongoza Stars kushinda mechi mbili nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco na kupoteza ugenini mbele ya Ivory Coast katika Kundi hilo la C.
Ubora wa Stars katika mechi hiyo ni katika kumiliki mpira na kutoa pasi zitakazowafanya kushambulia kwa urahisi wakati Morocco inategemea zaidi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na wengi wao wa kikosi cha kwanza wanacheza mpira wa kulipwa Ulaya.
Kwa upande wa maandalizi, Kim alisema Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imejiandaa vizuri kwani ilikuwa na kambi ya wiki moja nyumbani, wiki moja nyingine ikapiga kambi nchini Ethiopia, na baadaye hapa Marrakech ambapo pia imekuwepo kwa wiki nzima ikijiwinda kwa mechi hiyo.
Ikiwa nchini Ethiopia ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan iliyomalizika kwa timu hizo kutoka suluhu huku Kim akiwapa fursa ya kucheza wachezaji 16 akiwemo Haruni Chanongo aliyecheza dakika kumi za mwisho, ikiwa mechi yake ya kwanza baada ya kuitwa katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza.
Ndani ya miaka miwili, Stars itakuwa inakutana na Morocco kwa mara ya nne. Mwaka 2011 katika mechi za kutafuta tiketi ya Fainali za Kombe la Afrika mwaka 2012 nchini Afrika Kusini, Stars ilifungwa nje ndani (1-0 jijini Dar es Salaam na 3-1 jijini Marrakech).
Lakini katika mechi iliyopita Machi 24 mwaka huu Stars iliibuka na ushindi wa mabao 3-1,  yote yalifungwa kipindi cha pili. Shukrani kwa mabao hayo ya Mbwana Samata (mawili) na Thomas Ulimwengu.
Kim alisisitiza kuwa malengo yake kwa sasa ni kupigania nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia na kwamba timu yake imekuwa ikifanya vizuri kadri inavyoendelea kucheza ikiwa imeshafunga mabao matano katika mechi hizo za mchujo.
“Tulianza safari kwa kufungwa 2-0 ugenini na Ivory Coast. Katika mechi ile hatukupata bao na tukamaliza tukiwa kumi uwanjani baada ya mchezaji wetu mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu. Lakini kadri tunavyoendelea katika mashindano ndivyo timu inavyozidi kuimarika.
“Mechi hizi za Kombe la Dunia unatakiwa kushinda nyumbani zote, mipango ambayo kwetu bado inakwenda vizuri. Tukiwafunga Morocco kwao tutazidi kuimarika. Tunajua mechi itakuwa ngumu, nasi tumejipanga kwa hilo tukijua Morocco wanacheza nyumbani na watakuwa katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wao,” alisema Kim aliyeanza kuinoa Stars tangu Mei mwaka jana.

MATAJIRI WA YANGA KUMPA SHAVU BEKI WA SIMBA


In Summary
Chollo aliidengulia Simba kusaini mkataba mpya wiki iliyopita akishinikiza kupewa Sh.18 milioni, lakini Simba wakaachana naye na wakatumia fedha hizo kuwasainisha vijana wengine kama 12 hivi kutoka timu yao ya vijana.

YANGA bwana watata sana. Vigogo wa kamati yake ya usajili walitaka kuifanyia Simba rafu mbaya kwenye usajili wake lakini klabu ya Msimbazi ikashtuka na kuweka mambo sawa tena fastafasta.
Matajiri hao wa Jangwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin Kleb waliwahi kuifanyia Simba umafia msimu uliopita na kumnyaka beki tegemeo Kelvin Yondani na Mbuyu Twite.
Safari hii walipanga kufanya tena kwa beki Mzanzibari Nassor Masoud ‘Chollo’.
Chollo aliidengulia Simba kusaini mkataba mpya wiki iliyopita akishinikiza kupewa Sh.18 milioni, lakini Simba wakaachana naye na wakatumia fedha hizo kuwasainisha vijana wengine kama 12 hivi kutoka timu yao ya vijana.
Yanga waliposikia hivyo Jumanne iliyopita wakawasiliana na Chollo na Jumatano wakapanga kumaliza dili lakini ishu ikavuja kwa Simba.
Simba waliposikia, Jumatano wakamuita na kukubali kumpa kiasi alichokuwa akitaka na kwamba jana Ijumaa jioni alisaini mkataba mpya na kuachana na Yanga iliyopanga kumpa Sh.20 milioni.
Dili jipya alilopewa na Simba limemfanya apandishwe pia mshahara ambao utamuongezea utajiri mwaka huu.
Habari za ndani zinadai mchezaji huyo alikubali dau dogo la Simba kwavile alijua akienda Yanga uwezekano wa kumuweka benchi Mbuyu Twite ni mdogo na kwamba huenda akafulia kama Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’.
Chollo amekuwa akifanya mazoezi na Simba tangu Jumatano ingawa walimpa mpambe wa kufuatilia nyendo zake kuhakikisha hasaini Yanga.