Jumamosi, 8 Juni 2013

NI MDOGOLAKINI NI MACHACHARI


Beki huyo ameonyesha kuwa ni hodari wa kucheza mipira ya kichwa kwa kuzuia na kushambulia kutafuta mabao kama kona na krosi ingawa wasiwasi uliopo kwa mashabiki wa klabu hiyo ni udogo wa umbile lake.
 
UKIMUONA umbo lake unaweza kumuona wa kawaida sana, ni umbo ambalo halitishi. Si mrefu sana, si mpana sana ni mchezaji wa wastani tu, lakini shughuli yake isubiri uwanjani.
Mmoja wa wachambuzi mahiri na Mhariri wa Michezo wa Gazeti Kuu nchini Uganda la New Vision Fred Kaweesi alipoisoma Mwanaspoti na kusikia beki Samweli Ssenkoomi amesaini Simba alitamka maneno machache; “Simba wamepata mtu, huyo jamaa mzuri sana ila wasimpe presha bado mdogo sana. Wampe nafasi atumie akili yake.”
Simba imemsajili beki huyo wa Uganda kutoka URA kwa mkataba wa miaka miwili kwa lengo la kuimarisha safu ya beki ya kati ambayo iliyumba msimu uliopita na hata kwenye ripoti yake kocha aliyeachana na Simba, Mfaransa Patrick Liewig alishauri asajiliwe beki wa kati mzoefu. Alitua nchini usiku wa Jumatatu akitokea kwao Uganda na kuanza mazoezi ya pamoja na Simba Jumanne jioni wiki hii.
Akiwa katika mazoezi hayo, Ssenkoomi ameonyesha kuwa ni mjanja uwanjani na ana uamuzi wa haraka na uwezo mkubwa wa kupanda kushambulia mbele, pia ni mwepesi wa kushuka kuzuia.
Beki huyo ameonyesha kuwa ni hodari wa kucheza mipira ya kichwa kwa kuzuia na kushambulia kutafuta mabao kama kona na krosi ingawa wasiwasi uliopo kwa mashabiki wa klabu hiyo ni udogo wa umbile lake kwa sababu hamtishi straika ila ana akili na anajua anachokifanya.
Mwanaspoti ilizungumza naye akasema; “Nimeamua kuja Simba kwa lengo moja la kutimiza kile wanachokikusudia kwa kuhakikisha nacheza kwa ubora na kuifanya timu ing’are,”anasema Ssenkoomi ambaye anaishabikia klabu ya Real Madrid ya Hispania inayofikiria kumpa ukocha Zinedine Zidane.
“Lakini pia kwangu ni hatua moja, nina malengo ya kucheza Ulaya, kuja kwangu Simba nafungua njia kwa ajili ya kukamilisha ndoto zangu hizo. Naamini nitafanya kile ninachokikusuadia tena kizuri zaidi kubwa nahitaji ushirikiano kutoka kwa wachezaji wanzangu, benchi la ufundi na mashabiki kwa ujumla,”anafafanua Ssenkoomi aliyeweka wazi tayari amesaini mkataba wa miaka miwili na hakuja Tanzania kukaa benchi kwavile anataka kung’ara zaidi ya Joseph Owino beki wa Uganda aliyeondoka Simba.
Hata hivyo Ssenkoomi ametoa angalizo kwa kuwaomba mashabiki wampe muda kwani anatoka kwenye mapumziko na hajafanya mazoezi kwa kipindi kirefu.
“Ninatoka kwenye mapumziko, sijacheza kwa kipindi kirefu, ni ugumu ambao unanitatiza hata hivyo nitafanya kitu kitakachowafurahisha benchi la ufundi na mashabiki kwa ujumla,”anasema mchezaji huyo ambaye baada ya mazoezi ya kwanza na Simba alilalamikia uchakavu wa Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
“Kitu kingine ni ubovu wa sehemu ya kuchezea ndani, hali ya uwanja si nzuri imekuwa ikinipa wakati mgumu kucheza. Ushindani upo kila mahali, nimefurahi kukutana na wachezaji mbalimbali na kwa kipindi kifupi nimependa ushirikiano wao,”anasema na kuongeza kuwa amezoea mazingira ya Afrika Mashariki hivyo hadhani kama Tanzania itampa shida kwavile haitofautiani na Uganda.
“Wachezaji wazuri ambao kwangu ni changamoto na mambo mengine ni mimi mwenyewe katika kujituma, kufahamu majukumu yangu ninayopewa na mwalimu,” anaongeza mchezaji huyo ambaye Mwanaspoti linajua amependekezwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Simba, Mosses Basena ambaye ni raia wa Uganda.
Basena amewaambia viongozi kwamba mchezaji huyo ni mzuri na anaweza kufanya kazi kubwa kwenye ufundi ingawa habari za ndani zinadai kiungo wa TP Mazembe, Patrick Ochang anaomba kila kukicha arudi Msimbazi baada ya kupoteza namba katika kikosi cha wachezaji 18 wa kwanza Mazembe hivyo kumfanya kupoteza posho na masilahi manono.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni